Ajabu Kalonzo, Wamalwa kutishia kuondoka Azimio ilhali muungano uliisha zamani – Taifa Leo
Written by Black Hot Fire Network on November 6, 2024
TANGAZO la kiongozi wa chama cha Wiper Kalonzo Musyoka na mwenzake wa DAP- Eugene Wamalwa kwamba wataondoa vyama vyao kutoka Azimio La Umoja One Kenya lilitanguliwa na kusambaratika kwa muungano huo.
Japo unaweza kuwa upo kwa maandishi, ni wazi kuwa Azimio ilibaki gae baada ya chama kikubwa tanzu cha Orange Democratic Movement (ODM) cha aliyekuwa waziri mkuu Raila Odinga kujiunga na serikali.
Japo ODM inakanusha kuwa haina mkataba wowote wa ushirikiano na Serikali ya Kenya Kwanza, ni wazi kuwa kimo ndani huku wanachama wake wakiteuliwa mawaziri na wabunge wake wakiungana kutetea sera na mipango ya serikali inayopingwa na Wakenya wengi.
Hivi majuzi, chama hicho kilipinga baadhi ya miswada iliyotokana na ripoti ya pande mbili maarufu kama Nadco ambayo ingebuni Afisi ya Kiongozi Rasmi wa Upinzani Bungeni na kuanzisha wadhifa wa waziri mkuu.
Kamati ya pande mbili ilileta pamoja Azimio na Kenya Kwanza na kwa ODM kupuuza mapendekezo iliyochangia kuundwa kwake baada ya ukuruba wa kiongozi wake Raila Odinga na Rais William Ruto, ni wazi kuwa muungano huo wa upinzani ulikufa kitambo.
Iwapo ODM itaendelea kushikilia kuwa Azimio ipo, ni kwa kuwa inanuia kulinda nafasi za uongozi bungeni ambazo viongozi wake wanashikilia na zinawawezesha kupata minofu.
Kujiondoa kwa vyama Wiper na DAP- Kenya vinavyofuata nyayo za Narc Kenya cha Martha Karua, na Jubilee cha Uhuru Kenya kikifuata mkondo huo, basi itakuwa wazi Azimio ni sawa na maiti iliyo mochari ikisubiri mazishi rasmi kutangazwa.