Chepngetich alenga taji la mbio za kilomita 10 Romania – Taifa Leo
Written by Black Hot Fire Network on September 23, 2024
WAWANAWAKE saba kutoka Kenya akiwemo bingwa wa Michezo ya Afrika wa mbio za mita 10,000, Janet Chepngetich watashiriki mbio za kilomita 10 za tRUNsylvania zitakazofanyika mjini Brasov nchini Romania mnamo Septemba 22.
Chepngetich ni mmoja wa watimkaji wanaopigiwa upatu kutwaa taji.
Atawania tuzo ya Sh644,300 akikabiliwa na upinzani kutoka kwa Wakenya wenzake Loice Chemnung, Christine Njoki, Nelvin Jepkemboi, Judy Kemboi, Grace Loibach Nawowuna na bingwa wa Afrika, Gladys Kwamboka.
Pia, kuna Waethiopia Yeshaneh Anley, Lemlem Hailu, Lemlem Alemu, Godu Tekle na wazawa wa Kenya Daisy Jepkemei (Kazakhstan) na Stella Rutto (Romania).
Mojawapo ya majina makubwa katika kitengo cha wanaume ni mshindi wa medali ya fedha ya Olimpiki 5,000m, Ronald Kwemoi. Kwemoi atakutana na bingwa mtetezi Weldon Langat.
Rekodi za tRUNsylvania zinashikiliwa na Wakenya Sheila Kiprotich (dakika 30:07) na Nicholas Kimeli (26:51). Ziliwekwa mwaka 2022.
Wakenya Peter Aila na Nelly Jepchumba walishinda makala ya kwanza mwaka 2022 kwa 28:39 na 32:11, mtawalia.
Nambari mbili hadi nane watazawadiwa Sh322,325, Sh257,860, Sh193,395, Sh128,930, Sh103,144, Sh77,358 na Sh64,465, mtawalia.