Eric Omondi: Gen Z wamechukua breki, watarudi barabarani na kushinda

Written by on September 23, 2024


MCHEKESHAJI Eric Omondi amesema kuwa serikali ya Kenya Kwanza haifai kuchukulia kimya cha vijana wa Gen Z kuwa ushindi kwani watakuja na nguvu mpya.

Akizungumza Septemba 6, 2024 katika mojawapo wa mahojiano, mcheshi huyo ambaye amekuwa akitoa misaada mbalimbali kwa Wakenya wasiojiweza alisema kuwa serikali ya Kenya Kwanza ikiongozwa na Rais William Ruto haifai kusherehekea ushindi wa muda wa kuzima maandamano ya Gen Z.

“Usione mtu amenyamaza ukadhani ameshindwa. Vijana hao wako mapumzikoni, mchezo haujaisha. Huu mchezo tutashinda. Wakenya watashinda,’ akasema Bw Omondi.

Kando na hayo, Bw Omondi alisema kuwa kuna haja serikali kupunguza idadi ya magavana na wabunge.

Alisema kuwa hatua hiyo itaisaidia nchi katika kupunguza gharama na matumizi ya fedha.

Bw Omondi amekuwa kwenye mstari wa mbele wakati wa maandamano ya kupinga Mswada wa Fedha 2024 na hata wakati mwingine alipigwa na kukamatwa na polisi kwa kuandamana karibu na Jengo la Bunge la Kitaifa.

Amekuwa akiikosoa serikali ya Kenya Kwanza na kuishutumu kwa kupandisha gharama ya maisha nchini.

Kuna wakati alikuwa akigawa unga na hata kuwalipia Wakenya ambao hawajiwezi pesa ya matibabu kama njia ya kuonyesha umoja ya Wakenya.

Matamshi yake yanajiri wiki chache tu baada ya Kenya kushuhudia maandamano yaliyoleta mabadiliko makubwa nchini yaliyoanza Juni 18, 2024.

Maandamano hayo yalimlazimisha Rais Ruto kutupilia mbali Mswada wa Fedha 2024.

Baadaye, vijana hao waliendeleza maandamano kushinikiza kujiuzulu kwa Dkt Ruto na serikali yake.

Walidai aliruhusu kukithiri kwa ufisadi na mwenendo wa mawaziri kupuuza matakwa ya wananchi huku wakiweka wazi maisha yao ya anasa yaliyoonekana kutumia vibaya mali ya umma.

Kando na hayo, rais pia alilazimika kuwafuta kazi mawaziri wote 21, isipokuwa Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi.

Hata hivyo, walijitenga na maandamano hayo baada ya wahuni kuingilia kati na kuanza kupora mali ya Wakenya wakijifanya ni waandamanaji.



Source link


Reader's opinions

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *



Current track

Title

Artist