Gachagua akinyolewa, Mudavadi atahitaji kutia chake maji – Taifa Leo

Written by on October 1, 2024


NAIBU wa Rais Rigathi Gachagua angekuwa na chama chake chenye ushawishi katika eneo la Mlima Kenya, leo asingeangikwa ‘msalabani’ na wandani wa Rais William Ruto.

Masaibu yanayomwandama Bw Gachagua yanatokana na ukweli kwamba hana wabunge wa kumtetea. Idadi kubwa ya wabunge kutoka eneo la Mlima Kenya wanaegemea mrego wa Rais Ruto ambaye ni kiongozi wao wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Bw Gachagua sasa anaungwa na wabunge wasiozidi 10 – ambao wote wanatoka eneo la Mlima Kenya.

Katika ziara zake za kutafuta uungwaji mkono miongoni mwa wakazi wa Mlima Kenya wiki iliyopita, Bw Gachagua alikuwa akizunguka na wabunge wasiozidi wawili na madiwani wa zamani– ishara kwamba ameachwa mpweke.

Masaibu yanayokumba Naibu wa Rais Gachagua, yanafaa kumtia baridi kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi ambaye anapanga kuvunja chama chake cha Amani National Congress (ANC) na kujiunga na UDA.

Mnamo Juni, Bw Mudavadi alikubali kuvunja chama chake na kuingia UDA. Wajumbe wa ANC wakiongozwa na mwenyekiti wake Gavana Issa Timamy katika mkutano uliofanyika Ikulu ya Nairobi walikubali chama hicho kivunjwe. Kulingana na vigogo wa ANC, Bw Mudavadi atakuwa na nafasi nzuri ya kumrithi Rais Ruto iwapo atavunja chama chake na kujiunga na UDA.

Juhudi za kutaka ANC na chama cha Ford Kenya chake Spika wa Bunge Moses Wetang’ula kuvunjiliwa mbali zilianza mara tu baada ya uchaguzi wa 2022.

Mara baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa UDA, seneta wa zamani wa Kakamega Cleophas Malala, alianza kusukuma Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula kuvunja vyama vyao na kujiunga na chama tawala.

Dkt Ruto alifaulu kuhudumu muhula wa kwanza wa serikali ya Uhuru Kenyatta kati ya 2013 na 2017 bila kuhangaishwa kwa sababu alikuwa na wabunge wake wa chama cha United Republican Party (URP). Mnamo 2015, Rais Kenyatta na Dkt Ruto waliafikiana kuvunjilia mbali vyama vyao – URP na The National Alliance (TNA) – na kuunda chama kimoja cha Jubilee.

Baada ya kuchaguliwa kwa muhula wa pili, Rais Kenyatta ‘alipiga teke’ Dkt Ruto. Katika muhula wa pili wa Bw Kenyatta, Dkt Ruto alitengwa na alikuwa ‘mgeni’ serikalini.

Hivyo, Bw Mudavadi anafaa kufutilia mbali mpango wake wa kutaka kujiunga na UDA na badala yake akuze chama chake cha ANC ili kiwe na idadi kubwa ya wabunge katika uchaguzi ujao.

La sivyo, Bw Mudavadi atajipata kwenye baridi ya kisiasa kabla au baada ya uchaguzi wa 2027.



Source link


Reader's opinions

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *



Current track

Title

Artist