Ingwe yaendelea kung’aa Shabana ikibugia Tusker 4 kavu – Taifa Leo
Written by Black Hot Fire Network on February 12, 2024
Ingwe yaendelea kung’aa Shabana ikibugia Tusker 4 kavu
AFC Leopards jana iliendeleza wimbi la matokeo mazuri, huku Shabana ikinyeshewa 4-0 na Tusker kwenye mechi ya Ligi Kuu (KPL).
Mabingwa mara 12, Leopards walinyamazisha Murang’a Seal 1-0 ugani Nyayo, Nayo.
Nayo Tusker ilitamatisha kupoteza mechi mbili na kupiga Shabana katika uga wa Raila Odinga, Kaunti ya Homa Bay katika raundi ya 21.
Katika uwanja wa Police Sacco, Sofapaka walitoka sare ya 1-1 dhidi ya FC Talanta kwenye mechi ambayo ilianza mapema.
Baadaye ugani humo, Kakamega Homeboyz ilitamatisha wimbi la matokeo duni kwa kuzaba KCB 2-1.
Katika Kaunti ya Kisumu, wageni Kariobangi Sharks walizidishia Muhoroni Youth masaibu ya kushushwa ngazi kwa kuwachabanga 2-1 uwanjani Muhoroni.
Mjini Thika katika kaunti ya Kiambu, Nzoia Sugar ilipata ushindi wake wa nne msimu huu kwa kulima Bidco United 2-1.
Uwanjani Nyayo, Victor Omune alifunga kutoka kwa mpira wa kona uliochanjwa na winga Vincent Mahiga katika kipindi cha kwanza.
Kichapo hicho kilizima kidomodomo cha Seal ambao wamekuwa wakikejeli Ingwe wiki nzima kwa kukosa uwanja.
Ushindi huo ulihakikisha kuwa Leopards almaarufu Ingwe haijapoteza mechi katika michuano mitano mfululizo.
Ingwe ilipoteza mara ya mwisho mnamo Desemba 10 walipoangushwa 2-1 dhidi ya Bidco.
Ingwe imepanda hadi nambari saba kwenye jedwali. Ina alama 30 baada ya mechi 21.
Seal bado wapo nambari 12 kwa alama 24 licha ya kuanza msimu vizuri na hata wakati moja kuwa kileleni.
“Timu hii imeimarika sana na sisi ndio tulikuwa bora katika mechi hii. Ligi ya Kenya huwa ni ya wachezaji kutumia nguvu na mshambuliaji wetu Arthur Gitego atahitaji kuwa na uzoefu ndiposa bado siwaanzishi,” akasema kocha wa Leopards, Tomas Trucha.
Kocha wa Seal, Juma Abdallah alikiri kuwa wachezaji wake walifukuza vivuli kwa sababu Leopards wana uzoefu na walikuwa wamewazidi mbinu.
“Tulijaribu kufukuza mchezo huo, lakini tukashindwa. Lazima tujizatiti kuhakikisha kuwa tunajiandaa vyema kukabili timu mahiri ligini,” akasema.
Mabao ya Tusker dhidi ya Shabana yalifungwa na Deogratious Ojok, Ibrahim Joshua, Shaphan Oyugi na Joseph Mwangi. Tusker ilichapwa 1-0 na Bidco na Gor Mahia, mtawalia.