Kalonzo amevua taji la tiara wa kupeperushwa na upepo – Taifa Leo

Written by on November 14, 2024


KALONZO Musyoka anasalia kuwa mwanasiasa mwenye msimamo thabiti katika siasa za Kenya wakati huu. Baadhi ya watu wamedai kuwa yeye ni kigeugeu na wakamwita majina yanayomfanya kuwa vuguvugu.

Sifa hii inaweza kumfaa lakini nani mweupe kwa hilo katika siasa za Kenya? Raila Odinga anaweza kudhaniwa kuwa ana fikra za kimapinduzi ila hulka zake tangu 1997 zinaashiria kuwa ni mtu anayejali maslahi yake zaidi kuliko ya umma.

Kalonzo amekuwa na misimamo isiyoyumba kamwe na ameonyesha kwa dhati kwamba anataka kuwa Rais. Katika muungano wa Azimio, alijitangaza kuwa kiongozi baada ya Raila kutaka uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika.

Anajua hata kitabu kitakatifu kinasema ufalme haupatikani kwa kubahatisha, wanaouteka wanatumia nguvu. Martha Karua aliamua kujiondoa Azimio baada ya Raila kuanza usuhuba wa kisiasa na Ruto. Eugene Wamalwa naye yuasema pia paa la Azimio halimweki tena.

Kalonzo bado ameganda hapo. Hajali ikiwa washirika wake Jeremiah Kioni na Ferdinand Waititu wana misuli iliyonyong’onyea kisiasa.

Hatua ya baadhi ya wafuasi wa Kalonzo kumtaka kufanya kazi na aliyekuwa naibu Rais Rigathi Gachagua ni jambo linalostahili kumtisha Rais William Ruto hata ikiwa amemweka kwapani Raila Odinga.

Gachagua na masaibu yake bado anaweza kuufanya Mlima ama sehemu yake kumridhia Kalonzo.
Wabunge wengi wa Wiper walipiga kura katika bunge la taifa na seneti kumwokoa Gachagua. Walifuata maagizo ya Kalonzo, kiongozi wao.

Uungwaji mkono wa vijana wa Gen Z

Si hayo tu, Kalonzo ameonekana kuzingatia sana hoja na haja walizotoa vijana wakitaka mageuzi ya kitaasisi na sera za nchi. Kila wakati ikiwa umemsikiza vizuri, amekuwa akiwapongeza Gen – Z kwa kuiamsha serikali kutoka kwa usingizi wa pono. Hawa vijana wanaweza kuamua kushirikiana na Kalonzo kisha Ruto na washirika wake watapata taabu.

Kalonzo tangu aingie bungeni 1985 na kuondoka 2013, amehakikisha kuwa jamii ya Ukambani inakuwa gundi ya mshikamano. Wapinzani wake hawajafaulu bila baraka zake, waliojaribu walilambishwa sakafu kama Charity Ngilu alipojaribu useneta wa Kitui 2013. Pia alikuwa mgombea mwenza mtiifu kwa Raila Odinga mara mbili, 2013 na 2017.

Vigezo vingine vinavyoweza kumfanya Kalonzo kuwa chaguo bora ni kwamba, amewahi kuwa makamu Rais katika muhula wa mwisho wa Mwai Kibaki.

Na wanaorukaruka juu wakidhani Kalonzo ni mtu wa kijijini sana wafahamu kuwa aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na muafaka wa amani wa Sudan ulioafikiwa Naivasha 2005 alikuwa kiungo muhimu kujenga misingi halisi ya Sudan Kusini kuanza mchakato wa kuwa Jamhuri huru na kujitenga na Sudan.



Source link


Reader's opinions

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *



Current track

Title

Artist