Kinachomkoroga Gachagua Mlimani – Taifa Leo

Written by on September 23, 2024


NAIBU Rais Rigathi Gachagua ana wakati mgumu kutimiza masuala ambayo wakazi wa eneo la Mlima Kenya walitarajia ashughulikie, huku akikabiliwa na tishio la kutimuliwa afisini kupitia hoja bungeni.

Naibu Rais anatarajiwa kuanika changamoto za kisiasa ambazo zimemzonga kwa karibu miaka miwili tangu aingie afisini na jinsi atakavyokabiliana navyo, atakapohutubia wakazi wa kaunti za Mlima Kenya Jumapili, Agosti 4, 2024 kupitia vituo vya utangazaji vinavyotumia lugha za mama za eneo hilo.

Kwa mujibu wa mhadhiri wa chuo kikuu Profesa Macharia Munene, uwezekano wa Bw Gachagua kuteuliwa tena kama mgombea mwenza wa Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao wa 2027 ni finyu mno.

 

Bw Gachagua akifanya dua kwenye Mlima Kenya mnamo Machi 2023. PICHA | MAKTABA

“Anakabiliwa na shida kubwa zaidi kuliko mvutano wa ubabe kati yake na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi serikali. Sasa kiongozi wa upinzani Raila Odinga pia ameingia serikalini na anadhibiti wizara sita zenye ushawishi mkubwa, na bado atataka nyadhifa zaidi,” Prof Munene akasema.

Kuingia kwa Raila serikalini

Bw Odinga amefanya  wandani wake wakapewa nyadhifa za wizara za Fedha, Madini na Uchumi wa Baharini, Ustawi wa Vyama vya Ushirika, Kawi, Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, na Mwanasheria Mkuu.

Wakati Naibu Rais atakuwa akizungumza na wakazi wa Mlima Kenya – wanaojumuisha wanajamii wa Agikuyu, Aembu na Ameru – kwenye mahojiano hayo, wakazi hao watafuatilia kwa makini ili kusikiza majibu atakayotoa kuhusu masuala muhimu yanayoathiri maisha yao.

“Tutakuwa na hamu kujua nafasi yetu katika serikali hii tuliyoitundika mamlakani kwa kuipa asilimia 87 ya kura zetu, na hivyo kumpa rais uongozi wa nchi. Yule tuliyesukuma kwa upinzani ameletwa ndani na tunakubali. Kile tunataka kujua ni nafasi yetu imesalia nini,” akasema Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, mwandani wa karibu sana wa Bw Gachagua ambaye anaonekana kugeuka kuwa msemaji wake.

Bw Kahiga aliongeza: “Tunataka kujua jinsi tutakomesha malumbano ya kisiasa na kujikita katika shughuli za utoaji huduma, tukisubiri wakati Bw Odinga atajiondoa rasmi kwenye kinyang’anyiro cha urais 2027.”

Gavana huyo anamtaka Bw Gachagua kuondolea wakazi wa Mlima Kenya hofu kuhusu kuingia kwa Bw Odinga serikalini, hatua ambayo alisema imechangia umaarufu wa Rais Ruto kushuka Mlimani kiasi cha kuathiri azma yake ya kusaka kura tena eneo hilo kwa ajili ya uchaguzi wa 2027.

Vita dhidi ya pombe haramu

Naye Mbunge Maalum Sabina Chege alimshauri Naibu Rais anafaa kuongoza eneo hilo katika kampeni ya kutetea miradi ya maendeleo badala ya kujikita katika siasa za kuendeleza masilahi ya watu binafsi.

“Tuko katika hali ambapo yule nilijaribu kumsaidia kuukwea mlima lakini akashindwa, sasa ameingia serikalini. Sisi tuliomuunga mkono tulitajwa kama maadui. Sasa sote tuko serikalini na tunahimiza kupendana,” akaambia Taifa Leo mnamo Ijumaa, Agosti 02, 2024, katika eneobunge la Gatanga.

Diwani wa wadi ya Gatanga, Bw John Kibaiya, alisema eneo la Mlima Kenya linataka kusikia mbinu anazotumia Gachagua kuendeleza vita dhidi ya pombe haramu vinavyoonekana kulegea.

Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Agikuyu (Njuri Ncheke), Bw Wachira Kiago, anahoji kuwa Naibu Rais ana kibarua cha kuelezea wakazi hatua ambazo serikali imepiga kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo ambayo ni nguzo kuu ya uchumi wa Mlima Kenya.

“Tunataka kujua ikiwa tutaendelea kusubiri kuvuma matunda ya mageuzi katika sekta ya kilimo,” akasema.

Hatima ya Mt Kenya ndani ya UDA

Suala lingine ambalo wakazi wanataka kupata hakikisho kutoka kwa Bw Gachagua ni uthabiti wa kisiasa na kukomesha kwa mivutano isiyo na maana.

“Aidha, tunataka kujua nafasi yetu katika chama cha UDA tulichosaidia kuunda,” akasema Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya.

Kwa upande wake Mbunge wa Naivasha Jane Kihara alisema suala la uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pia ni lenye uzito mkubwa kwa wakazi wa Mlima Kenya.

Naye Seneta wa Kiambu Karungo Wa Thang’waa alisema wakazi wa Mlimani wanataka kujua ni lini mfumo wa ugavi wa mapato wa “mtu mmoja-kura moja-shilingi moja” utaanza kutekelezwa.



Source link


Reader's opinions

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *



Current track

Title

Artist