Kuria amejisogeza kwa Raila lakini wafuasi wafaa kumpuuza, anasaka ‘uhai’ kisiasa – Taifa Leo
Written by Black Hot Fire Network on November 11, 2024
VIONGOZI wa ODM wanastahili kujihadhari na wanasiasa kama vile Moses Kuria ambao wanalenga tu kutumia Kiongozi wa Upinzani Raila Odinga kwa manufaa yao lakini ikifika wakati wa kura wanambagua na kurejea kwa makabila yao.
Nilifuatilia hotuba ya Bw Kuria wikendi wakati wa hafla ya kusherehekea uteuzi wa Gavana wa Homa Bay Gladys Wanga kama mwenyekiti wa ODM, Kaunti ya Homa Bay. Niliona dalili thabiti za hadaa za siasa.
Bw Kuria alisimama jukwaani akiwa amevaa kofia ya ODM na kudai kuwa katika mwaka wa 2027 kutakuwa na muungano ambao unafanana na ule wa Narc wa 2002 ambao ulimuingiza mamlakani Rais Mwai Kibaki (sasa marehemu).
Aliendelea kujipiga kifua kuwa mnamo 2018 alibashiri kuwa Bi Wanga angekuwa gavana wa Homa Bay na kuwa wakati akihudumu kama waziri wa Viwanda, ndiye wa kwanza kuleta viwanda vya kisasa katika kaunti hiyo na Siaya.
Kilicho wazi ni kuwa hizi ni siasa za kujizolea umaarufu na kutaka huruma kutoka kwa watu ambao Bw Kuria mwenyewe amewahi kuwatusi na kuwadhihaki ili atimize maslahi na ajenda zake za kisiasa.
Huyu ndiye kiongozi ambaye baada ya uchaguzi wa mnamo 2022 pamoja na Mbunge wa Mbeere Kusini Geoffrey King’ang’i walielekea Mahakama ya Juu kupinga kesi ambayo Raila alikuwa amewasilisha kupinga ushindi wa Rais William Ruto.
Katika kesi yao walilaumu Raila na Azimio la Umoja kutokana na fujo na utata uliozingira matokeo ya urais kwenye ukumbi wa Bomas.
Huyu ndiye kiongozi ambaye kwa sasa anatumia jukwaa la kisiasa Homa Bay kujipendekeza kwa jamii ambayo amekuwa akimtusi kiongozi wake na kuwaita maneno yasiyochapishika.
Ni jambo ambalo liko wazi kuwa Bw Kuria amewahi kunyakwa kwa kutoa matamshi ya uchochezi na kikabila dhidi ya Raila na wafuasi wake wakati wa utawala wa Jubilee.
Je, wakati huo hakujua kuwa atakuja kumhitaji Raila ili waunde muungano wa kisiasa wa 2027?
Kwa miaka miwili ambayo Bw Kuria alikuwa waziri, alifanyia nini wakazi wa Nyanza kiasi kuwa sasa aje na kuanza kubashiri kuwa atakuwa na muungano nao kuelekea kura za 2027?
Aliwaajiri wangapi katika wizara yake? Miradi aliyodai alianzisha ya viwanda vya kisasa Siaya na Homa Bay vimefikia wapi na vimenufaisha nani?
Siasa ambazo Kuria alicheza Homa Bay ni hadaa tupu wala hafai kuchukuliwa kama kiongozi ambaye atanufaisha wafuasi wa Raila kivyovyote kiasi cha kuhitaji muungano nao.
Kinachomsumbua Bw Kuria ni kujipata kwenye baridi baada ya kutimuliwa kama waziri. Hili linachangiwa hasa na Raila kutumia ushawishi wake kuanzisha ushirikiano na Rais William Ruto hali iliyoishia baadhi ya wandani wake kuingia serikalini.
Wadhifa ambao alipewa kama mshauri wa rais kuhusu masuala ya kiuchumi ni mdogo ikilinganishwa na uwaziri na sasa anasaka njia ambayo atatumia kujikwamua kisiasa kwa kuwatumia wafuasi wa Raila ambao amekuwa akiwachukia kwa miaka mingi.
Bw Kuria yuko huru kucheza siasa zake lakini afahamu kuwa watu wamegutuka na wanaelewa janjaure zake. Chuki za kikabila na dharau ambazo amewahi kuonyesha wafuasi wa Raila zinatosha kutia tashwishi.