Mlima umerejea ulikokuwa kisiasa katika miaka ya ‘90 – Taifa Leo
Written by Black Hot Fire Network on November 26, 2024
MATUKIO ya kisiasa yanayoendelea ukanda wa Mlima Kenya yanaonyesha kuwa eneo hilo limerejea mahali lilikokuwa mwanzoni mwa mfumo wa siasa za vyama vingi mapema miaka ya 90.
Aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua amefaulu kujitwalia umaarufu eneo hilo na kumnyima kabisa Rais William Ruto ufuasi wa ukanda huo kuelekea kura za 2027.
Mlima Kenya haujawahi kuwa katika hali ambayo umejipata kisiasa tangu 2002 ambapo umekuwa serikalini 2002, 2007, 2013, 2017 na 2022.
Wikendi iliyopita, matukio mawili yalishuhudiwa Murang’a ambapo wakazi walikataa kusomewa hotuba ya Naibu wa Rais Prof Kithure Kindiki katika hafla ya mazishi ya aliyekuwa diwani katika Kaunti ya Murang’a.
Aliyekuwa waziri wa Utumishi wa Umma Moses Kuria alizomewa na waombolezaji na kuzuiwa kuhutubu huku hotuba ya Rais Ruto nayo ikikosa kusomwa na kukabidhiwa familia kutokana na upinzani wa raia.
Mnamo Jumapili, kulikuwa na umati mkubwa ambao haujawahi kushuhudiwa hivi karibuni uliohudhuria mkutano mkubwa wa kisiasa katika uwanja wa Ihura ambapo raia walionyesha uaminifu wao kwa Bw Gachagua.
Wiki moja iliyopita, Rais Ruto alizomewa katika Kaunti ya Embu wakati wa kusimikwa kwa askofu wa Kanisa la Katoliki Peter Kimani.
Aidha, Gavana wa Embu alijipata pabaya kwa kukashifu kuzomewa kwa Rais na kujaribu kutenga Mlima Kenya Mashariki na Mlima Kenya Magharibi.
Bi Mbarire aliambiwa kuwa wakazi wa Mlima Kenya ni wamoja na wote wako nyuma ya Bw Gachagua.
Itakumbukwa kuwa wakati wa maandamano ya Gen-Z, Mlima Kenya ni kati ya maeneo ambayo maandamano yalichacha na afisi ya Bi Mbarire pia ilichomwa na waandamanaji wenye hasira.
Maasi yaliyopo dhidi ya serikali kwa sasa yalishuhudiwa Mlima Kenya ulipoanza kuasi uongozi wa Rais Daniel arap Moi baada ya Mwai Kibaki kujiondoa serikalini mnamo 1988 na Kenneth Matiba kumfuata kwenye upinzani.
Wakati wa mapambano ya mfumo wa vyama vingi, Mlima Kenya wote ulikuwa nyuma ya Bw Matiba ambaye alishirikiana na vigogo wengine kama Charles Rubia, Kibaki, Kiraitu Murungi na Gitobu Imanyara miongoni mwa wanasiasa wengine. Wakiendeleza uanaharakati huo, kulikuwa na wanasiasa wengine ambao walikuwa wakishabikia serikali kama J J Kamotho, Joshua Angaine, Njenga Karume miongoni mwa wengine ambao walikuwa mrengo wa serikali.
Bw Gachagua amefaulu kuwa kama Matiba leo huku Profesa Kindiki ambaye alichukua pahala pake sasa akionekana kama Karume na Kamotho wa jana akirejelewa kama msaliti.
Siasa za Mlima Kenya huongozwa na chuki wala si sera au uchapakazi wa viongozi na kwa utawala wa sasa, hasira ipo zaidi kutokana na kutimuliwa kwa Bw Gachagua na ahadi za maendeleo zisizotimizwa.
Katika kura za 2013 walipiga kura kwa fujo kuzuia Kinara wa upinzani Raila Odinga kupata uongozi wakati ambapo Uhuru Kenyatta alikuwa akiandamwa na kesi katika Mahakama ya Jinai ya ICC.
Mnamo 2022 walipiga kura kumwaadhibu Uhuru na Raila ambao walikuwa wakishirikiana kisiasa.
Kwenye kura za 2007 na 2017 walipiga kura kusalia mamlakani na mnamo 1992 na 1997 msingi wao wa kupiga ulikuwa kupata mamlaka.
Ifikapo 2027 kuna uwezekano mkubwa watapiga kura kumwaadhibu Rais Ruto na ni dhahiri mkondo ambao Bw Gachagua atafuata ndio watakaoukumbatia.