Saum inavyomkurubisha mja na Mola wake – Taifa Leo
Written by Black Hot Fire Network on March 14, 2025
KWA jina la Mwenyezi Mungu mwenye kuneemesha neema kubwa kubwa na neema ndogo ndogo. Alhamdulillahi.
Sifa na shukrani zote zimwendee Muumba wetu, Mwenye-Enzi ambaye ametujaalia neema chungu nzima. Neema ya kuwa waumini wa dini hii tukufu ya Kiislamu.
Neema ya kufaidi uhondo wa mwezi huu mtukufu wa Ramadhan. Neema ya kuwa hai na kutekeleza ibada mbali mbali. Na neema nyinginezo kedekede.
Sisi waumini wa dini ya Kiislamu tunapokuwa kwenye ibada yoyote ile tunajua wazi kuwa hiyo ndiyo njia ya kumkaribia Mola wetu.
Tunapokuwa kwenye swala, tunapotoa sadaka, tunapotoa zaka, tunapofunga, tunapoleta dhikr, tunapotendeana wema, na kila aina ya ibada, basi tunakuwa karibu na Mola wetu.
Tunazungumza naye. Ndiyo maana kwenye funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhan tunapata jukwaa mwafaka la kunena moja kwa moja na Allah (SWT). Na kumkaribia kabisa.
Hili limejitokeza wazi kwenye kitabu chetu kitukufu cha Kurani sura ya Al-Baqarah aya ya 186: “Na waja wangu watakapokuuliza hakika yangu, (waambie kuwa) Mimi niko karibu nao. Naitika maombi ya mwombaji anaponiomba. Basi na waniitikie na waniamini, ili wapate kuongoka.”
Hebu fikiria ewe ndugu yangu muumin ambaye upo kwenye mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan ni kwa namna gani utukufu wa ibada ya funga ya saumu unavyotukurubisha na Allah (SWT).
Funga ya saumu ambapo hata baadhi ya swala za sunna unahesabiwa kuwa ni faradhi. Ibada ambayo malipo na jaza yake ajuaye ni Mola pekee.
In Shaa Allah saumu itukurubishe na Mola wetu.