Wakenya walivyotawala mbio za Trunsylvania nchini Romania – Taifa Leo
Written by Black Hot Fire Network on September 23, 2024
WATIMKAJI Loice Chemnung na Daniel Kinyanjui waliendeleza utawala wa Kenya kwenye mbio za kilomita 10 za tRUNsylvania mjini Brasov nchini Romania mnamo Septemba 22.
Chemnung alitia mfukoni Sh644,300 baada ya kuibuka mshindi wa kitengo cha kinadada kwa dakika 30 na sekunde 13.
Kinyanjui pia alipokea kitita hicho baada ya kulemea mpinzani wake wa karibu kutoka Morocco kwa sekunde 0.01 akitwaa taji la wanaume kwa dakika 27:08.
Chemnung alifuatiwa kwa karibu na bingwa wa Michezo ya Afrika mbio za 10,000m Janeth Chepngetich (30:19), nao Judy Kemboi (30:29), Grace Loibach (30:33), Nelvin Jepkemboi (30:34) na Christine Njoki (30:36) wakafunga sita-bora katika usanjari huo.
Katika kitengo cha wanaume, Kinyanjui alimaliza mbele ya Mmoroko Hicham Amghar (27:09), huku Wakenya Weldon Langat (27:09), Daniel Kimaiyo (27:15), Patrik Mosin (27:20), Benard Langat (27:24), Abraham Kipyatich (27:29) na Victor Mutai (27:30) wakifuatana kutoka nafasi ya tatu hadi sita, mtawalia.
Wakenya Peter Aila na Nelly Jepchumba walivuna mataji ya mwaka 2021 kwa 28:39 na 32:11, nao Sheila Kiprotich na Nicholas Kimeli wakashinda makala ya pili mwaka 2023 kwa rekodi ya dakika 30:07 na 26:51, mtawalia.
Hapo Jumapili, nambari mbili hadi nane walituzwa Sh322,325, Sh257,860, Sh193,395, Sh128,930, Sh103,144, Sh77,358 na Sh64,465, mtawalia.