Wanaume wanakufa na ukimwi kuliko wanawake licha ya maambukizi machache – Taifa Leo
Written by Black Hot Fire Network on November 18, 2024
WANAUME wengi hapa nchini wanaaga dunia kutokana na virusi vya ukimwi na magonjwa yanayoandamana na virusi hivyo ikilinganishwa na wanawake.
Takwimu kutoka Baraza la Kitaifa la Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukizana (NSDCC) zinaonyesha kuwa zaidi ya watu milioni 1.38 wana ukimwi huku wanaume wakiwa ni asilimia 35 (487,710). Hii ni licha ya kuwa wanaume wachache ndio wanaishi na virusi hivyo.
Licha ya kuwa idadi ndogo ya wanaume ndiyo huambukizwa ukimwi (asilimia 2.2) ikilinganishwa na wanawake (asilimia 4.5), wanaume ndiyo huaga dunia kutokana na virusi hivyo hatari.
Mnamo 2023, wanaume 26 walikufa kila siku kati ya idadi ya vifo 56 ambavyo vilitokea kila siku kutokana na ukimwi na magonjwa mengine yanayoandamana na virusi hivyo.
Naibu Mkurugenzi wa NSDCC Caroline Kinoti alisema wanaume ndio hufa kutokana na virusi hivyo kwa sababu huwa hawaendi hospitalini na hilo husababisha virusi kuwa na nguvu zaidi kisha kupanda hadi viwango vya juu.
Hawaendi hospitalini
“Kinyume na wanawake ambao huenda hospitalini wakiwa na mimba na hupimwa ukimwi, wanaume huenda tu hospitalini wakilemewa na maradhi. Hapa ndipo wao hubainika wana ukimwi japo wakiwa wamechelewa,” akasema Bi Kinoti wakati wa warsha na wanahabari Machakos mnamo Ijumaa.
Ingawa hivyo, idadi ya wanaume ambao wanatumia vidonge vya ARVs imepanda kutoka asilimia 81 mnamo 2020 hadi asilimia 90 mnamo 2023. Wanaume pia hukumbana na changamoto za matumizi ya dawa za kulevya, uhalifu na pia huwa hawashiriki mipango ya afya ya kuzuia maradhi mbalimbali,” akaongeza Bi Kinoti.
Mnamo 2023, Kenya ilikuwa na maambukizi mapya 16, 752 za ukimwi huku wanaume wakiwa 4,072. Watu ambao wapo katika umri wa kati ya 15-34 walijumuisha asilimia 73 za maambukizi yote, wanaume wakiwakilishwa kwa idadi ya juu kwenye tapo hilo.
Ingawa hivyo, wanaume ndio waliaga dunia kwa idadi ya juu kwa mujibu wa takwimu hizo za NSDCC na kuwakilisha asilimia 48 ambayo ni vifo 9,808. Hii ni licha ya kuwa ni theluthi ya wanaume ndiyo walikuwa wakiishi na virusi hivyo mnamo 2023.
“Tofauti hii kubwa ni kutokana na afya iliyodorora kwa sababu wanaume huwa hawaendi kupokea matibabu, huchelewa kufanya vipimo vya ukimwi na hawafuati maagizo ya daktari wakati wa matibabu,” akasema Bi Kinoti.
Makali ya virusi
“Hii ndiyo maana wanaaga dunia kwa idadi ya juu kutokana na makali ya virusi.”
Japheth Kioko pia kutoka NSDCC alifichua kuwa maambukizi mapya yamepungua sana tangu 2023. Mwaka jana, zaidi ya Wakenya 16,572 waliambukizwa ukimwi wengi wakiwa matineja na vijana kati ya umri wa miaka 15-34.
Huu ni upungufu wa watu 5,000 kutoka 22,154 ambao walikuwa wameambukizwa mnamo 2022. Bw Kioko alisema kuwa wanawake 8,937 walipatikana na virusi vya ukimwi mwaka jana ikilinganishwa na wanaume 4,072 na watoto 3743 ambao wapo chini ya umri wa miaka 14.
Kaunti za Kisumu, Homa Bay, Migori, Siaya, Nairobi, Nakuru, Kiambu, Busia na Mombasa ndizo zilichangia asilimia 51 za maambukizi mapya ya ukimwi mwaka jana.