Yote unayopaswa kufahamu kuhusu gonjwa hili – Taifa Leo

Written by on September 23, 2024


ULIMWENGU umemakinika zaidi kuhusu aina mpya ya virusi vya homa ya nyani (Monkey pox – Mpox) ambavyo vimezidi kusambaa Afrika na kupenya kwa mara ya kwanza Uropa baada ya kuripotiwa nchini Sweden.

Wataalam wametaja aina mpya ya virusi vya mpox kama iliyo hatari zaidi huku Shirika la Afya Duniani (WHO) kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka miwili, likitangaza mlipuko unaoendelea kuwa dharura ya afya ya umma duniani.

Kufikia sasa mwaka huu, visa 2,863 vimethibitishwa huku vifo 517 vikirekodiwa huku ikikikadiriwa kuna jumla ya visa 17,000 vya mpox.

Mataifa ambayo hayajawahi kuathiriwa na gonjwa hili ikiwemo Kenya, Uganda, na Rwanda, yameripoti virusi vya mpox.

Mpox ni nini?

Mpox ilifahamika awali kama homa ya nyani. Ni maambukizi ya virusi vinavyopatikana sanasana Afrika Magharibi na ya Kati.

WHO ilibadilisha jina la homa ya nyani 2022 ili kuondoa ‘lugha ya ubaguzi wa rangi na unyanyapaa’ unaohusishwa na gonjwa hilo.

Mpox husambazwa vipi?

Binadamu aliambukizwa gonjwa hili kwa kutagusana na kuchakulo wanaoaminika kubeba virusi hivyo.

Kuchakulo ni wanyama wenye viwele, ambao hunyonyesha wanao.

Mpox inafahamika pia kama maambukizi ya zinaa kwa sababu huambukizwa kupitia mtagusano wa karibu na mtu anayeugua, hususan kujamiiana.

Kutagusana ngozi kwa ngozi, kushiriki malazi, mavazi au taulo na mtu aliye na virusi hivyo.

Mpox ilianzia wapi?

Kisa cha kwanza kiliripotiwa Congo kabla ya maambukizi kurekodiwa Afrika Magharibi na ya Kati.

WHO ilitangaza mlipuko wa virusi vya mpox kuwa dharura ya afya ya umma kufuatia mlipuko uliozuka Amerika na Uropa ambapo mashoga waliathirika zaidi.

Aina mpya ya virusi

Aina mpya ya virusi (Clade 1b) ilipozuka Septemba 2023, imetokana na aina hatari zaidi ya mpox (Clade1) inayotofautiana na (Clade 2) aina ya kwanza ya virusi vya mpox.

Maambukizi kupitia ngono kwa mara nyingine yamehusishwa pakubwa na usambazaji wa aina mpya ya virusi vya mpox.

Visa vya kwanza viligunduliwa miongoni mwa wachuuzi wa ngono katika mji wa uchimbaji madini wa Kamituga, Congo, takriban maili 170 kutoka mpaka wa Rwanda.

Kihistoria, virusi aina ya Clade 1, hupatikana miongoni mwa watu wanaokula wanyama wa porini walioambukizwa ambapo maambukizi aghalabu hujikita katika familia husika.

Dalili za mpox

Dalili za mpox huanza kama homa, maumivu ya kichwa, viungo, mgongo, uvimbe kwenye nyonga, shingo, makwapa na uchovu.

Baada ya siku tano, upele huanza kujitokeza kuanzia usoni kisha unasambaa kote mwilini ikiwemo sehemu nyeti.

Vipele hivyo vinafanana na vya tetekuwanga na huanza kama sehemu zilizovimba zinageuka chunusi zilizojaa usaha kabla ya kuwa makovu yanayoanguka.

Japo visa vingi hutokomea kivyake bila hata matibabu, mpox, inayoweza kudumu hadi kwa mwezi mmoja, inaweza kusababisha vipele vya mara kwa mara kote mwilini, kupofuka na hata kifo.

Virusi vipya vinahusishwa na asilimia tano ya vifo miongoni mwa watoto na asilimia 10 kwa watu wazima.

Idadi kubwa ya “mimba kutoka” vimeripotiwa miongoni mwa wanawake wajawazito wanaoambukizwa mpox.

 



Source link


Reader's opinions

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *



Current track

Title

Artist